Rais John Magufuli
Hayo yalibainishwa jana na katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue, wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu kuhusu siku 100
za Rais Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Balozi Sefue aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kutokana na
hatua kubwa na nzuri alizochukua Rais Magufuli kupambana na maovu na
kujenga uchumi wa nchi, "wako watu wameonesha wazi kutamani tungewaazima
Rais Magufuli aongoze nchi zao kwa muda."
Sefue alisema Sh. bilioni 7 zilizookolewa zingeweza kutumika kwa
safari za nje iwapo safari za nje zilizokuwa zimezoeleka zisingepigwa
marufuku na Rais wa tano.
Mwishoni mwa mwaka jana, Ofisi ya Rais ilisambaza mwongozo unaoweka
masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi
watatakiwa kutimiza ili wapewe kibali cha kusafiri, ikiwa ni pamoja na
kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Ofisi za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba
12 ikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje ya
nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake.
Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.
Ili kuonyesha kuwa tamko la kupiga marufuku safari hizo halikuwa la
mzaha, watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), waliosafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu walisimamishwa
kazi.
Waliosimamishwa kazi ni watumishi waandamizi wa taasisi hiyo
akiwemo Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, Mary Mosha, Ekwabi Mujungu
na Rukia Nikitas.
Kwanini Rais Magufuli hajasafiri nje ya nchi siku 100 Ikulu?
Sefue alibainisha kuwa tofauti na wanaomlaumu Rais kwa kutosafiri
nje ya nchi, yeye anafahamu na kushukuru kuwa Marais waliomtangulia
walifanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga uhusiano wa Tanzania na nchi za
nje na kuimarisha diplomasia na mataifa hayo.
Alisema Rais anatambua kuwa ili ailinde sifa hiyo, na kuikuza,
lazima anyooshe mambo kadhaa ndani ya nchi kwani iwapo Tanzania itabaki
kuwa maskini, yenye rushwa, ujangili, madawa ya kulevya na kadhalika,
hiyo sifa nzuri nje ya nchi itaporomoka.
“Rais ameamua kujipa muda kuimarisha uchumi na maendeleo ndani ya
nchi, na kupambana na matatizo mengine yanayoharibu sifa yetu, ili iwe
rahisi kudumisha sifa ya Tanzania nje ya nchi," alisema Balozi Sefue.
"Wengi mtakubaliana nami kwamba hatua anazochukua Rais Magufuli
kuimarisha mifumo na utendaji wa humu ndani, umeipa sifa kubwa Tanzania
huko nje pamoja na kwamba yeye binafsi hajasafiri kwenda nje ya nchi
tangu achaguliwe kuwa Rais.”
Alisema hiyo inadhihirisha wazi kuwa mambo ya ndani
yasiposhughulikiwa ipasavyo, kusafiri tu kwa Rais nje siyo kigezo cha
kudumisha heshima na urafiki mwema.
“Napenda niwahakikishie wananchi wote kuwa dunia inafuatilia
yanayotokea nchini, na wanashahuku ya kuona matokeo yake maana kila kona
hivi sasa, nchi zinazungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano
ndani ya siku 100.
"Hili ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na nchi za nje na ni jambo kubwa kidiplomasia.”
Aidha, Sefue alisema fedha zilizookolewa kwenye sherehe za siku ya
Ukimwi zimekwenda kununua dawa za kufubaisha makali ya virusi vy Ukimwi,
wakati fedha ambazo zingetumika kwenye semina elekezi ya Mawaziri,
zitakwenda kutekeleza mradi wa kufunga vifaa vya kisasa vya kuchunguza
magonjwa katika hospitali 37 kote nchini.
Mbali na kuokoa kiasi hicho cha fedha, Sefue alisema serikali ya
awamu ya tano ndani ya siku 100 za kwanza imefanikiwa kuongeza makusanyo
ya kodi na mapato yasiyo ya kodi.
Alisema katika kipindi cha siku 100 za kwanza, mapato ya kodi
yameongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 3.34, ikilinganishwa na
makusanyo ya Sh. trilioni 2.59 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha
2014/15, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 746.31.
Hali kadhalika, Sefue alisema kwa mapato yasiyo na kodi, makusanyo
yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 281.68, kutoka Sh. bilioni 224.03
katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Sh.
bilioni 57.65.
“Nyote mmesikia, baada ya kashikashi pale Hospitali ya Taifa
Muhimbili, mapato yao yameongezeka maradufu na kuwapa uwezo mkubwa zaidi
wa kuhudumia wananchi.
"Hali ni hiyo pia kwenye Halmashauri kwani ukusanyaji huu wa mapato
umeiwezesha Serikali kugharamia baadhi ya miradi yake kwa fedha za
ndani, mathalan, kuwalipa wakandarasi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi
ya maji, miundombinu, umeme, kilimo, uwezeshaji wa vijana na
kadhalika.”
Kuhusu nidhamu serikalini, Sefue alisema tayari serikali imepata
mrejesho kutoka kwa wananchi kuwa nidhamu kwenye utumishi wa umma
imeongezeka na wananchi wanahudumiwa kwa haraka zaidi, na kwa heshima
zaidi.
Alisema serikali ya Magufuli imedhamiria kurejesha nidhamu ya kazi
na kutokomeza utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha na
kwamba katika tafsiri pana zaidi, hatua hizo zinalenga kukuza utamaduni
wa uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uhodari, bidii na ufanisi
mkubwa, kunakoendana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
“Ndiyo sababu Rais aliwalisha kiapo cha uadilifu Makatibu Wakuu na
Naibu Makatibu Wakuu wote aliowateua na kamwe watumishi wa umma
wasisahau kuwa wao ni watumishi, sio mabwana, wa wananchi wawatumikie
kwa ufanisi, kwa uaminifu na kwa heshima kubwa,” alisisitiza Sefue.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni